Habari Mkuu wa 246 Online!
Hali ya uchumi imekaza, na wengi wetu tunatamani kumiliki simu kali—iPhone X, Samsung S-Series, au Google Pixel—lakini bei za dukani (mpya ndani ya box) zinatisha. Suluhisho la wengi ni kukimbilia simu za "Used from UK/Dubai" au mitumba iliyotumika hapa hapa bongo.
Lakini ukweli mchungu ni huu: Soko la simu used Tanzania limejaa "Mabomu". Kuna wajanja wengi wako tayari kukuuzia simu iliyochoka, iliyoibiwa, au "Clone" (Feki) kwa bei ya simu original. Ukishatoa pesa, imekula kwako!
Kabla hujaenda dukani na pesa zako za mawazo, 246 Online tumekuandalia Checklist ya Kijasusi. Haya hapa ni mambo 5 unayopaswa kuyafanya hapo hapo dukani mbele ya muuzaji kabla hujamkabidhi hela.
Usiingizwe chaka, twende kazi... π§π
1. Usiangalie Kioo Tu: Kagua "Body" Kizushi
Wauzaji wengi hubadilisha vioo vilivyopasuka na kuweka vipya ili simu ionekane mpya (Refurbished). Usidanganyike na ung'avu wa kioo.
- Cha kufanya: Angalia pembeni mwa simu (kwenye fremu) na nyuma. Je, kuna mikwaruzo mikubwa au alama za kudondoshwa? Simu iliyopigwa chini sana inaweza kuwa na matatizo ya ndani (motherboard) ambayo yataanza kukusumbua baada ya wiki moja.Kidokezo: Angalia "screws" (nati ndogo) chini ya simu karibu na sehemu ya kuchajia. Zikionekana zimeshikwa shikwa sana au zimelegea, jua hiyo simu imefunguliwa mara nyingi. Kuwa makini!
2. Muhimu Sana: Hakiki IMEI Namba (Kujua Original vs Feki)
Hapa ndipo wengi wanapopigwa. Simu inaweza kuandikwa "Samsung S22 Ultra" kwa nje, lakini ndani ikawa ni simu ya Tecno ya zamani iliyobadilishwa jina.
- Cha kufanya:
- Fungua sehemu ya kupiga simu, piga
*#06#. - Simu itaonyesha namba ndefu inaitwa IMEI. Iandike pembeni au uishike kichwani.
- Zima simu, thibitisha kama IMEI iliyoandikwa nyuma ya simu (kama ipo) au kwenye "Sim Card Tray" inafanana na hiyo uliyoiona kwenye kioo.
- Level ya Juu: Ukiwa bado dukani, tumia simu nyingine kuingia kwenye website kama IMEI.info. Ingiza hiyo namba. Ikikuletea majina tofauti na simu unayotaka kununua (mfano unanunua iPhone inaleta Nokia), kimbia! Hiyo ni feki.
3. Mtihani wa "Secret Menu" (Kukagua Vifaa vya Ndani)
Hujui kama spika inafanya kazi vizuri, au kama "touch" ya kioo imekufa upande mmoja? Usibahatishe. Kila simu ina menu ya siri ya mafundi ya kukagua hivyo vitu.
- Kwa Android (Samsung, n.k): Piga
*#0*#(Au baadhi ya simu ni*#*#4636#*#*). - Itafunguka menu yenye viboksi vingi. Bonyeza kimoja kimoja: Jaribu Touch (upitishe kidole kioo kizima), jaribu Speaker, jaribu Vibration, na Sensor. Hakikisha vyote vinaitika.
- Kwa iPhone: Haina code ya moja kwa moja, lakini tumia app ya "Voice Memos" kurekodi sauti yako na kuisikiliza (kupima mic na spika). Shika icon yoyote kwenye home screen na uizungushe kioo kizima kuhakikisha "Touch" haikatiki sehemu yoyote.
4. Afya ya Betri (Battery Health) - Ugonjwa Mkubwa!
Hakuna kitu kinakera kama simu inayozima ikiwa na chaji 30% au inayolika chaji kama maji.
- Kwa iPhone: Nenda Settings > Battery > Battery Health.
- Ikionyesha chini ya 80%, jua hiyo betri imechoka na utahitaji kuibadilisha hivi karibuni. Hiyo ni sababu ya kuomba kupunguziwa bei. Ikionyesha "Service", usinunue kabisa.
- Kwa Android: Simu nyingi hazionyeshi hii asilimia moja kwa moja. Angalia jinsi asilimia zinavyoshuka ukiwa unaikagua hapo dukani. Kama ndani ya dakika 5 za kuichezea imeshuka 10%, hilo ni tatizo.
5. Mtego wa "iCloud" na "Google Lock" (FRP)
Usinunue simu ambayo bado ina "Account" ya mwenyewe wa zamani. Hata wakikwambia "tutakutolea baadae", KATAA.
- Cha kufanya: Kabla hujalipa, mwambie muuzaji aifanye simu iwe Factory Reset (Wipe Data) mbele yako.
- Ikimaliza kuwaka, jaribu kui-set up kama simu mpya. Ikiomba email ya zamani (iCloud au Google Account) ambayo muuzaji haijui, hiyo simu ni "Kimeo" au imeibiwa. Usiichukue hata bure, itakufia mkononi.
HITIMISHO
Kununua simu used ni njia nzuri ya kuokoa pesa, lakini inahitaji ujanja. Usione aibu kuikagua simu kwa muda mrefu hapo dukani. Hela ni yako na una haki ya kupata kitu kizuri.
Kama muuzaji anakuzuia usiikague kwa undani, jua ana kitu anaficha. Ondoka zako.
Save hii post na share na mshkaji ambaye anapanga kwenda kununua simu "mpya" hivi karibuni umuokoe na majanga!
Maoni